Mapendekezo ya ripoti ya CAG kwenye zabuni za umma yachagize uwajibikaji

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Mussa Juma Assad (Photo by Mwananchi online)
Na: Nelson Kessy (Afisa Mahusiano, PPRA)
Katika toleo la wiki iliyopita tulichapisha makala iliyokuwa inatoa changamoto kwa wataalam wa manunuzi katika serikali za m mitaa kujifunza kutoka kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG). Aidha, makala hiyo ilijikita zaidi katika mamlaka za serikali za mitaa 171, na yalionesha kuwa taasisi 50 zilikiuka sheria ya manunuzi ya umma katika michakato ya manunuzi. Makala ya leo itaongelea umuhimu wa kuzingatia mapendekezo yaliyotolewa na CAG katika ripoti yake hiyo ya mwaka wa fedha 2015/16.

Ripoti hiyo imeweka wazi kuwa ni vyema taasisi zilizokaguliwa kuhakikisha zinazingatia matakwa ya sheria ya manunuzi, hasa katika eneo la uandaaji na utekelezaji wa mpango wa mwaka wa manunuzi, ambapo zinapaswa kuwasilisha kwa  Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) mipango ya manunuzi ya mwaka na ripoti za utekelezaji wa manunuzi. Jambo hili ni matakwa ya sheria na huchangia katika kuongeza uwazi na uwajibikaji.
Pia ripoti imeonyesha kuwa katika taasisi nyingi kulikuwa na manunuzi yaliyofanywa bila kuidhinishwa na bodi ya zabuni.
Mara nyingi manunuzi ya aina hii huwa ya gharama kubwa na pengine kuwa viashiria vya rushwa ambapo ni kinyume na Sheria ya Manunuzi ya Umma Kifungu cha 104 (2) (c) pamoja na Kanuni Namba 20 na 70. Suala la ukaguzi na upokeaji wa bidhaa/huduma na manunuzi kutoka kwa wazabuni walioidhinishwa ni jambo muhimu sana kwani bila kufanya hivyo taasisi inaweza kupokea bidhaa au huduma zilizo chini ya kiwango hali ambayo itaisababishia Serikali hasara kinyume na Kanuni Namba 245 ya kanuni za manunuzi ya umma za mwaka 2013.
 Aidha, wakati mwingine vifaa au huduma hununuliwa kwa bei ya juu kuliko ile ya soko pamoja gharama kubwa zinazotokana na uendeshaji wa michakato.
Changamoto nyingine ni pale taasisi za umma zinapokubali kupokea kutoka kwa wazabuni bidhaa au huduma zisizo na ubora au miradi iliyotekelezwa chini ya kiwango. Hata hivyo, taasisi zikizingatia mapendekezo ya CAG zitaisadia Serikali kukamilisha majukumu yake kwa wakati na kwa ufanisi.
Uadilifu katika vitengo vya manunuzi, bodi za zabuni na mamlaka nyingine zinazohusika na manunuzi, ni jambo muhimu. Pamoja na sheria kuweka bayana umuhimu wa kuzingatia misingi ya uadilifu na uwajibikaji, bado sekta hii inakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo vitendo vya rushwa, udangayifu pamoja na ubadhilifu.


Katika kuhakikisha Serikali inafanya manunuzi yenye ufanisi, PPRA imekuwa ikiaandaa mfumo maalumu wa usimamizi wa taarifa za manunuzi unaofahamika kama Procurement Management Information System - PMISambapo mfumo huu unatumiwa na taasisi nunuzi kuwasilisha taarifa mbalimbali za manunuzi PPRA kwa urahisi na kwa wakati. 

Hivyo, ni matarajio yangu kuwa ripoti ya CAG itatumika kama chachu ya kujirekebisha na kuweza kuleta ushindani, uwazi, uwajibikaji pamoja na matumizi sahihi ya fedha za  umma  yenye kuzingatia upatikanaji wa thamani bora ya fedha.

Comments

Popular posts from this blog

Mzabuni zingatia haya unapojaza nyaraka za zabuni, wengi hukosa kwa vigezo hivi

Marekebisho Sheria ya Manunuzi ya Umma Yanavyochagiza Tanzania ya Viwanda

Hatua anazopaswa kuchukua mzabuni asiyeridhishwa na mchakato wa utoaji zabuni