MAKALA: Waandishi wa habari ongezeni ‘wino’ kwenye manunuzi ya umma

Picha na planetminecraft.com
Na: Joseph Muhozi
Kwanza niwapongeze waandishi wa habari nchini kwa kazi nzuri wanayoifanya kuwahabarisha wananchi kuhusu mambo muhimu yenye maslahi ya umma katika sekta mbalimbali nchini. Nikiwa kama sehemu ya wana taaluma wa habari, natambua changamoto ziliko mbele yetu, lakini bado waandishi wengi wamekuwa wakitanguliza mbele maslahi ya umma.

Tumekuwa tukishuhudia kazi nzuri ya vyombo vya habari kwa ujumla wao sio tu katika kuuhabarisha umma, bali pia kuelimisha umma kadiri iwezekanavyo kwa kufanya uchambuzi rahisi kuhusu bajeti ya serikali punde inaposomwa bungeni.

Pia, kazi nzuri kama hiyo kwa kiwango cha kuridhisha hufanywa pale inapotoka ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), na pale inapotoka ripoti ya ukaguzi unaofanywa na Mamlaka ya Manunuzi ya Umma (PPRA). 

Hata hivyo, kwa kuzingatia kwamba wanahabari wanalo jukumu la kitaaluma la kuwajibika kwa umma na kuwa walinzi makini wa maslahi ya umma dhidi ya wahujumu wa fedha za mlipa kodi hususan, kwa kuhuisha uwazi utakaoleta uwajibikaji kwenye sekta ya manunuzi ya umma, nachelelea kusema kuwa kazi hiyo inayofanywa na waandishi wa habari haitoshi kwa manunuzi umma ambayo huchukua zaidi ya nusu ya bajeti ya Serikali. Ingawa zipo pia juhudi za waandishi ambao walipelekea kuibuliwa kwa baadhi ya mambo yaliyofanyiwa kazi kikamilifu na vyombo husika.
Lakini waandishi wa habari wanapaswa kuongeza nguvu katika kuripoti kuhusu michakato ya manunuzi ya umma na usimamizi wa mikataba husika, kuhakikisha kuna ‘uwazi’ kwenye michakato ya manunuzi kama sheria ya manunuzi ya umma inavyoelekeza. Hiyo itapelekea kuokoa fedha nyingi za walipa kodi zinazopotea kutokana na kukosekana kwa uwazi unaozaa uwajibikaji.

Kwa mfano, kwa mujibu wa ripoti ya PPRA ya Tathmini ya Utendaji kwa Mwaka wa Fedha 2015/16, kutokana na kukosekana kwa uwazi kwenye manunuzi ya umma, pamoja na mapungufu mengine ya udhaifu kwenye michakato na usimamizi wa mikataba, serikali ilipata hasara ya shilingi bilioni 23.41, huku ripoti hiyo ikitaja uwepo wa viashiria vya rushwa kwa kiwango kikubwa.

Ni rai yangu kwa vyombo vya habari kutoishia kuripoti matokeo haya na upotevu mkubwa wa fedha za umma, badala yake vijikite zaidi katika kutekeleza wajibu wa kuwa ‘walinzi wa mali za umma’, kwa kufuatilia nakuibua harufu za ukiukwaji wa sheria ya manunuzi ya umma kwenye michakato na utekelezaji wa mikataba husika.

Kwa bahati nzuri, sheria ya manunuzi ya umma inataka michakato ya manunuzi ya umma kufanyika kwa uwazi. Hivyo, mwandishi anaweza kuifuatilia tenda husika kuanzia wakati wa utangazaji wake, upatikanaji wa mshindi, namna atakavyotekeleza mkataba na ubora wa mradi husika.

Kutoa taarifa mapema za uwepo wa ukiukwaji wa sheria katika michakato ya manunuzi ya umma hupelekea PPRA kusitisha mchakato, kufuta mchakato, kuanzisha ukaguzi maalum dhidi ya mradi husika na kuwachukulia hatua wahusika, hivyo kuokoa fedha za umma kabla ya kuziweka kwenye ripoti kama sehemu ya hasara ilisobabishwa na watendaji wasio waaminifu.

Kwa asiye mtaaluma wa habari, wakati mwingine anaweza kujiuliza ‘nitawezaje kufahamu kuwa pale kuna ukiukwaji wa sheria katika manunuzi ya umma’. Lakini kwa waandishi wa habari tunafahamu kuwa ni lazima tuwe na sifa ya kuwa na uwezo wa kunusa habari (nose for news). Uwepo wa usiri katika mchakato husika pia ni sehemu ya harufu ya uwepo wa ukiukwaji wa sheria.
Katika hatua nyingine, PPRA kwa kutambua umuhimu wa waandishi wa habari katika sekta ya manunuzi ya umma, ilifanikisha uanzishwaji wa kipengele cha manunuzi ya umma katika Tuzo za Umahairi wa Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT), lakini kwa miaka miwili mfululizo (2015 na 2016) tuzo hiyo imekosa mshindi.
Hali hii ni kiashiria cha uwepo wa kiwango kisichoridhisha cha uwasilishaji bora wa habari za manunuzi ya umma kwa wananchi, kinachofanywa na vyombo vya habari  nchini.
Hata hivyo, PPRA imeendelea na juhudi za kuwaelimisha waandishi kuhusu sheria ya manunuzi ya umma kwa kutoa mafunzo maalum kwenye mikoa mbalimbali.
“Tunafahamu kumuelimisha mwandishi wa habari ni sehemu ya kuhuisha ‘uwazi’ katika manunuzi ya umma. Hivyo, tangu mwaka juzi, Mamlaka kupitia program maalum imekuwa ikitoa mafunzo maalum kwa waandishi wa habari ili waweze kusaidia katika kufuatilia kwa ukaribu michakato ya manunuzi ya umma na kuuelimisha umma. Lengo ni kushirikiana katika kuhakikisha tunapata thamani bora ya fedha kwenye manunuzi ya umma,” alisema Mcharo Mrutu, Afisa Mahusiano Mwandamizi wa PPRA.
Ni dhahiri kuwa katika kufanikisha hili, waandishi wa habari wanahitaji kupata ushirikiano kutoka kwa taasisi nunuzi, wazabuni na wananchi kwa ujumla wao ili wao wasaidie kupaza sauti kwa vyombo husika.
Kwa kutambua umuhimu huo, hivi karibuni, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe aliwataka watumishi wa umma (maafisa wenye dhamana ya kutoa taarifa za taasisi) kutoa ushirikiano kwa vyombo vya habari, huku akiahidi pia kuweka utaratibu wa ofisi yake kukutana na waandishi wa habari angalau kila mwezi ili kujadili na kutafuta ufumbuzi wa changamoto za upatikanaji wa habari katika ofisi za umma.
Hivyo, Taasisi nunuzi pia zina wajibu wa kuhakikisha waandishi wanapata majibu ya maswali yanayohusu michakato ya manunuzi ya umma na utekelezaji wa mikataba husika, bila kuvunja sheria na taratibu za utumishi wa umma.
Nimalize kwa kusema kuwa, waandishi wa habari tuzitumie fursa za mafunzo yanayotolea na PPRA kupata elimu zaidi kuhusu sheria ya manunuzi ya umma, na ikiwezekana tuhangaike zaidi kuchukua hatua za kufanya ufuatiliaji katika michakato ya manunuzi ya umma na kuanika maovu kabla hasara haijapatikana.

Kama ilivyo kwa sekta nyingine, Tanzania kuna fursa kubwa ya waandishi wa habari kusomea masuala ya manunuzi kwa lengo la kuwa waandishi wabobezi wa habari za manunuzi ya umma, sekta inayochukua zaidi ya nusu ya bajeti yote ya serikali. Mwandishi anaweza kujielemisha hata katika ngazi ya cheti au stashahada kisha kuisoma vizuri sheria ya manunuzi ya umma, ubobezi huu utapelekea kukoreza zaidi wino wa mwandishi katika habari za manunuzi ya umma katika kuhakikisha lengo kuu la kupata thamani bora ya fedha kwenye manunuzi ya umma linafikiwa. Pia, tuzo za EJAT zitakuwa na ushindani mkubwa zaidi wa wenye vigezo husika. 

Comments

Popular posts from this blog

Mzabuni zingatia haya unapojaza nyaraka za zabuni, wengi hukosa kwa vigezo hivi

Marekebisho Sheria ya Manunuzi ya Umma Yanavyochagiza Tanzania ya Viwanda

Hatua anazopaswa kuchukua mzabuni asiyeridhishwa na mchakato wa utoaji zabuni